Blog

  • UTAJIRI WA KIMUNGU NDANI YAKO

     “Maana mwaijua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba alikuwa maskini kwa ajili yenu, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”

     2 Wakorintho 8:9

    Wakristo wengi humtafuta Mungu kana kwamba bado wanajaribu kumshawishi awabariki. na wakati Neno la Mungu linatufundisha tofauti kabisa, kwamba kupitia kazi ya Yesu Kristo msalabani, tayari tumepokea urithi mkuu ndani yake (Utajiri). Yesu alijitoa kwa ajili yetu ili tuingie katika utajiri wa neema yake na urithi wa ahadi zote ambazo Baba ameweka kwa watoto wake.

    Hii inamaanisha kuwa kabla hatujaona matokeo katika ulimwengu wa mwili, Mungu tayari ameweka ndani yetu uwezo, neema, hekima, vipawa na ahadi zinazohitajika ili tuishi maisha yenye ushindi na utajiri.  Na ili Kile kilichopo katika ulimwengu wa roho kiweze kudhihirishwa katika maisha yetu ya kila siku, basi hatuna budi ila kutembea katika utii kwa Roho Mtakatifu na kufanya kazi kwa bidii.

    Roho Mtakatifu hutuelekeza kupitia Neno la Mungu. Mara nyingi maelekezo yake yanahusisha kufanya kazi kwa bidii, kutumia vipawa vyetu kwa uaminifu, kuwa waadilifu, kujifunza, kuhudumia wengine kwa ubora, na kusimamia vizuri kile ambacho Mungu ametukabidhi. na kila wakati tunapotii maelekezo hayo kwa imani, tunafungua nafasi ya kuona kile ambacho Mungu ameweka ndani yetu kikionekana katika maisha yetu.

    Ndiyo maana ni muhimu kuwa na mtazamo wa kiimani kuhusu utajiri. Mtu anayeamini kwamba Mungu amemwandalia urithi wa baraka hufanya maamuzi tofauti katika mambo ya kila siku ukilinganisha na yule asiye amini.  Hataongozwa na hofu au mawazo ya upungufu, bali atatafuta maarifa, atafanya kazi kwa bidii, atatumia muda wake kwa hekima, atawekeza katika ukuaji wake, na atatafuta fursa ambazo Mungu anafungua mbele yake. Imani hubadilisha jinsi tunavyofikiri, na jinsi tunavyofikiri huathiri maamuzi tunayofanya kila siku.

    Usikubali kuishi kwa mtazamo wa umaskini wakati Mungu amekuita kutembea katika utajiri wa neema yake. Amini kile ambacho Mungu amesema kuhusu wewe, fuata maelekezo ya Roho Mtakatifu kupitia Neno lake, na fanya kazi kwa bidii na uaminifu. Kadiri unavyotembea katika maelekezo ya Roho mtakatifu na kufanya kazi kwa bidii ndivyo utakavyoona urithi ambao Mungu ameweka ndani ya Kristo ukizidi kudhihirika katika maisha yako. Barikiwa.

  • FANYIA KAZI WOKOVU WAKO

    Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana nisipokuwapo, ufanyeni kazi wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.”

    Wafilipi 2:12

    Mara nyingi wakristo wengi hukubali kuishi maisha ambayo yako chini sana ya kiwango ambacho Mungu amewaandalia. Wanaridhika na ushindi mdogo, maarifa madogo ya Neno la Mungu, maisha ya kawaida ya kiroho, na matokeo yasiyoakisi urithi wao ndani ya Kristo Yesu. Lakini Mungu hakutuita tuokoke na kubaki mahali pamoja, katika uchache na udogo; badala yake alituita tukue, tumjue zaidi, na kuingia katika utimilifu wa ahadi zake.

    Ndio maana Mtume Paulo alipowaandikia Wafilipi aliwahimiza “kuufanyia kazi wokovu wao.” Hii haimaanishi kwamba wokovu hupatikana kwa matendo yetu,La ! kwa maana tunaokolewa kwa neema kupitia imani katika Yesu Kristo. lakini badala yake, inamaanisha kwamba baada ya kuokolewa tunapaswa kujitoa kwa bidii katika kumtafuta Mungu, kulitii Neno lake, na kuruhusu maisha yetu yaonyeshe kile ambacho Mungu tayari ameweka ndani yetu.

    Mungu ameweka ahadi nyingi kwa watoto wake. Ameahidi uponyaji, utajiri, amani, nguvu, hekima, ushindi, ulinzi, neema, na urithi wa kiroho ulio mkuu ndani ya Kristo yesu.

     Hata hivyo, ahadi hizi hazipaswi kupuuzwa au kuachwa zikiwa kama maandishi ya kawaida tu. Badala yake tunapaswa kuzisoma, kuziamini, kuzitamka kwa imani, na kuziombea mpaka zionekane katika maisha yetu.

    Kuufanyia kazi wokovu wako kunamaanisha kukataa kuridhika na kiwango cha chini cha maisha ya kiroho. Na kufanya uamuzi wa kutumia muda katika maombi, kujifunza neno la Mungu, kujenga ushirika wa karibu na Mungu, na kusimama imara juu ya ahadi zake, hata pale mazingira yanapoonekana kupingana nazo. Kadiri unavyomtafuta Mungu kwa bidii, ndivyo unavyozidi kutambua utajiri wa urithi wako ndani ya Kristo na kuanza kuuishi.

    Leo, fanya uamuzi wa kutokukubali maisha yaliyo chini ya kile ambacho Mungu amesema kuhusu wewe. Mungu anakualika usonge mbele, ukue kiroho, na uingie katika utimilifu wa kila ahadi aliyokuwekea. Wokovu wako ni mwanzo wa safari, si mwisho wake.

    Endelea kuufanyia kazi kwa kumtafuta Mungu kwa moyo wote, na utaona utukufu wake ukidhihirika katika kila eneo la maisha yako. Barikiwa.

  • USIISHI CHINI YA KIWANGO

    (Ishi Maisha Bora Aliyokuwekea Mungu)

    “Maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba alikuwa tajiri, lakini kwa ajili yenu alifanyika maskini, ili ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” — 2 Wakorintho 8:9

    Moja ya mambo ambayo adui amekuwa akipambania ni kuwafanya waamini wengi wakubali kuishi maisha yaliyo chini ya kiwango ambacho Mungu amewaandalia. Wengi wameokoka, wanampenda Mungu, lakini bado wanaishi chini ya ahadi, uwezo, na urithi waliopokea ndani ya Kristo Yesu.

    Andiko letu la utangulizi linatukumbusha gharama kubwa ambayo Yesu alilipa kwa ajili yetu. Yesu, aliyekuwa tajiri katika utukufu wa mbinguni, alikubali kujinyenyekeza na kubeba umaskini wetu ili sisi tuwe washiriki wa utajiri wa neema yake. Hii inamaanisha sio lazima kuishi maisha ya umasikini tena.

    Ndugu mpendwa siku zote kumbuka hili hupaswi kuridhika kuishi maisha ya kushindwa wakati Kristo Yesu ameshinda kwa ajili yako. Hapaswi kukubali kuishi katika umasikini wala kukubali kukaa mbali na ahadi za Mungu wakati umefanywa mrithi pamoja na Kristo.

    Mungu ana kiwango cha maisha alichokuandalia ndani ya Kristo. Kiwango hicho si cha wastani, si cha kushindwa, wala si cha kukata tamaa. Ni maisha ya ushindi, baraka na utajiri mwingi. Lakini ili kufikia kiwango hicho, ni lazima umtafute Mungu kwa bidii, ujifunze Neno lake kwa uaminifu, na udumu katika maombi. lazima uwe na SHAUKU ya kufikia ahadi za Mungu.

    Usikubali kufungwa na mazoea ya zamani, mazingira yako ya sasa, au maneno ya watu. Kile Mungu amesema kuhusu wewe kina uzito kuliko kile ambacho dunia inasema. Endelea kumtafuta Mungu, kwa maana ndani yake kuna kila kitu unachohitaji ili kuishi maisha bora aliyokuwekea.

    Barikiwa.

  • UTAMBULISHO WAKO MPYA NDANI YA YESU KRISTO

    (Wewe ni mrithi wa ahadi za Mungu Pamoja na Yesu)


    “Na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate kutukuzwa pamoja naye.” — Warumi 8:17

    Mtu anapomwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wake, hupokea maisha mapya na utambulisho mpya.Utambulisho huo mpya haujengwi juu ya historia yako, makosa yako, mafanikio yako, au maoni ya watu kuhusu wewe. Utambulisho wako huu mpya wa sasa umejengwa juu ya kile ambacho Yesu Kristo amekufanyia pale msalabani. Ndani ya Yesu, wewe ni watoto wa Mungu, aliyebarikiwa, aliyependwa, na aliyekombolewa. Na ukumbuke kuwa Kabla ya wokovu, ulikuwa mtumwa wa dhambi na mtu aliyekuwa mbali na Mungu. Lakini kwa neema yake, Mungu amekupokea katika familia yake na kukufanya mtoto wake yaani mrithi wa ahadi zake.

    Warumi 8:17 inafundisha kwamba kuwa mtoto wa Mungu kunakupa nafasi ya kuwa warithi wa ahadi zake. Na kwa vile warithi hupokea kile ambacho baba yao amewaandalia, basi vivyo hivyo, Mungu amekuwekea ahadi nyingi kupitia Yesu Kristo. Ahadi hizi ni pamoja na uwepo wake daima ndani yako, uponyaji, baraka, amani inayopita ufahamu, nguvu za kushinda majaribu, Pamoja na uzima wa milele.

    Hivyo shujaa wa Bwana ni muhimu kuelewa kuwa sasa wewe upo ndani ya Yesu na hivyo ina maanisha kuwa hakuna adui anayeweza kukugusa wewe kabla ya kumgusa Yesu, lakin pia wewe sasa ni mrithi wa ahadi zote za Mungu pamoja na Yesu, hivyo unapoona mambo

    haya endi kama unavyotaka basi simama kwa maombi na udai kilicho chako.

    Barikiwa.

  • KUONGOZWA NA ROHO

    KUONGOZWA NA ROHO

    “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.”

    Rumi 8:14

    Kwa kusema ukweli mimi ninapenda sana safari, hususani safari za mbali na nyumbani kuelekea mahali ambapo sijafika bado. Lakini na kupenda safari  kote huko, ninapokuwa mahali ambapo sipafahamu kabisa ( yaani ugenini) ninapenda kuongozana na mwenyeji wangu maana nikiwa naye ninajua kuwa siwezi kupotea njia kamwe.

    Vivyo hivyo na sisi katika safari yetu hii ya maisha ya baraka na ushindi ndani ya Yesu Kristo tunaye mwenyeji wetu,yaani  Roho Mtakatifu, ambaye yeye anayo kazi ya kutufikisaha kwenye uelewa kamili wa kila jambo ( yaani kutuongoza kufikia mafanikio ). HIvyo basi kama unataka usipotee njiani bali ufikie kila ahadi iliyowekwa kwa ajili yako katika neno la Mungu basi mshirikishe Roho wa Mungu (kwa maombi) kila hatua unayopitia. Na yeye kwa vile ni mwaminifu atakuongoza kwa kukupa hekima ya kukusaidia kufikia ushindi daima. Barikiwa.

  • HEKIMA YA MUNGU

    “ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;”

    Waefeso 3:10

    Tokea zama za kale Mungu amekuwa akitaka kuonesha uweza wake kwa viumbe vyote kupitia wanadamu. Mfano Mungu alionesha uweza wake kwa kupasaua bahari ya Shamu wakati wa Musa, pia alitoa maji kutoka mwambani na hata kuwalisha watu zaidi ya 5000 chakula kutokana na Samaki wawilI na mikate mitatu tu.

    Na sasa Mungu anataka kuoesha sio nguvu tu bali pia na hekima yake ya ajabu, na ndio maana akalichagua kanisa kuwa jukwaa lake la maonesho…..

    “ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho.”

    Waefeso 3:10

    Na hekima ya Mungu ni hii kuwa kwa milele yote shetani ameshashindwa, yaani haiajalishi anafanya lipi ila mwishho wake litaishia katika kushindwa tu. Lakini pia hekina nyingine ambayo Mungu anataka kuionesha kwetu ni kuwa kwa kumwamini kwetu Yesu tumefanyika Watoto wa Mungu na hivyo tumekuwa na haki za ahadi mbalimbali. Ahadi ambazo zinaweza kufanya maisha yetu kuwa bora zaidi kiafaya na kiuchui.

    Kwa hiyo mtu wa Mungu ni jukumu lako kuonesha kwa watu wote hekima hii ya kimungu kuwa sisi ni washindi katika mambo yote na shetani ni wa kushindwa milele yote. Barikiwa.

  • DUNIANI KAMA MBINGUNI

    “Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”

    Mathayo 6:10

    Kuna baadhi ya watu kwa kutokujua wamekubaliana na uongo wa shetani kwamba Mungu anawataka wao waishi maisha ya umasikini na taabu nyingi hapa duniani cha msingi waende Mbinguni tu. Huo ni uongo.

    Katika sala maarufu ya BABA YETU Bwana Yesu alitufundisha kuwa kumbe ni mapenzi ya Mungu sisi yaani mimi na wewe tuishi hapa duniani kama Mbinguni. Piga picha kama vile Mbinguni kusivyokuwepo na umasikini vivyo hivyo na kwako kusiwepo na umasikini, kama vile mbinguni kulivyo na makazi mazuri basi pia ni mapenzi ya Mungu hapa duniani wewe na mimi tuishi katika makazi mazuri. Ni lazima uziamini Habari hizi maana kwa kuamini utaweza kudai haki zako za baraka (Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo…..Mithali 10:22), na hivyo kukuwezesha wewe kuishi hapa duniani kama Mbinguni. Barikiwa.

  • UZIMA KATIKA MUNGU

    “……………..Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”

    1 Yohana 3:8

    Haijalishi ni ugonjwa wa namna gani iwe ni mdogo kama kuumwa Kichwa tu au mkubwa kama saratani bado ugonjwa ni kazi ya ibilisi( Shetani), na maandiko yanatuonesha kuwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita Bwana na mwokozi wetu YESU aliziharibu kazi zake.

    Hivyo nataka utambue kuwa magonjwa hayana haki ya kuwepo mwilini mwako, na kama kwa namna yoyoyte ile unasumbuliwa na ugonjwa wowote sasa ndio wakati wa kuuamuru kwa jina la Yesu utoke kwako, maana maandiko yanatuonesha kuwa

    “ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;
    Wafilipi 2:10

    Unapo amuru ugonjwa kuondoka kwako kwa jina la Yesu basi kuwa na Imani kwamba lazima utaondoka tu maana hakuna kazi ya ibilisi inayoweza kupinga mamlaka ya jina la Yesu. Simamia neno la Mungu na udai uzima wako maana ni mapenzi ya Mungu kwako uwe na afya njema na mwenye maisha ya furaha. Barikiwa.

  • IMANI NA UPENDO

    “Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.”

    Wagalatia 5:6

    Katika kila jambo kuna utaratibu wa namna mambo yanavyo paswa kufanyika ili kutoa matokeo yanayokusudiwa. Na kama ilivyo katika ulimwengu wa mwili vivyo hivyo katika ulimwengu wa roho kuna utaratibu wa namna mambo yanafanyika.

    Mungu wetu ameweka ahadi kubwa mno za thamani kwa kila mtu, ahadi hizi zinalenga kutuwezesha kuishi maisha ya usalama, furaha, afya na mafanikio tele. Lakini ili tuweze kuzipata hizo ahadi ni lazima kutumia Imani.  Na ili Imani ifanye kazi ni lazima kuwepo na UPENDO. Ndio maan andiko la utangulizi

    likasema  “…….bali imani itendayo kazi kwa upendo.”

    Ndugu mpendwa Upendo kwa Imani ni kama Mafuta katika gari, pasipo upendo Imani haitofanya kazi. Na kama Imani haitofanya kazi basi hauwezi kupokea ahadi za Mungu kwako. Kwa hiyo kama unataka kufurahia yale mengi ambayo Mungu ameweka kwa ajili yako basi hauna budi bali kuenenda katika Imani na upendo kwa watu wote. Barikiwa.

  • UMUHIMU WA IMANI

    “ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.”

    Waebrania 6:12

    Unajua katika ulimwengu wa biashara kinachotofautisha bidhaa bora na nyinginezo, ni faida anayoipata mtumiaji, na ndio maana kuna baadhi ya bidhaa hata kama ni za gharama kubwa kiasi gani lakini bado huwa hazikosekani majumbani mwetu, na yote ni kwa sababu tu ya  faida zake kwetu.

    Vivyo hivyo na kumpokea YESU kuna faida zake katika maisha yetu ya kila siku, baadhi ya faida zake huyu YESU ni uponyaji wa magonjwa na baraka tele. Sasa japokuwa kuna faida nyingine nyingi sana ukiacha hizo mbili zilizotajwa hapo juu, lakini watu wengi hawanufaiki na faida hizo, na sababu kuu ni kukosa Imani.

    Na ndio maana neno likasema

    “ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa IMANI na uvumilivu.”

    Waebrania 6:12

    Mtu wa Mungu kuna faida nyingi ndani ya Yesu, faida ambazo zinaweza kufanya maisha yako yakawa ya furaha na mafanikio hapa duniani lakini itakugharimu kuishi kwa Imani. Kumbuka neno la Mungu linasema kuwa

    “Mwenye haki ataishi kwa Imani……. Rumi 1:17” Barikiwa.

Design a site like this with WordPress.com
Get started