Author: Mwl.Daudi Mwarizo

  • IMANI NA UPENDO

    “Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.”

    Wagalatia 5:6

    Katika kila jambo kuna utaratibu wa namna mambo yanavyo paswa kufanyika ili kutoa matokeo yanayokusudiwa. Na kama ilivyo katika ulimwengu wa mwili vivyo hivyo katika ulimwengu wa roho kuna utaratibu wa namna mambo yanafanyika.

    Mungu wetu ameweka ahadi kubwa mno za thamani kwa kila mtu, ahadi hizi zinalenga kutuwezesha kuishi maisha ya usalama, furaha, afya na mafanikio tele. Lakini ili tuweze kuzipata hizo ahadi ni lazima kutumia Imani.  Na ili Imani ifanye kazi ni lazima kuwepo na UPENDO. Ndio maan andiko la utangulizi

    likasema  “…….bali imani itendayo kazi kwa upendo.”

    Ndugu mpendwa Upendo kwa Imani ni kama Mafuta katika gari, pasipo upendo Imani haitofanya kazi. Na kama Imani haitofanya kazi basi hauwezi kupokea ahadi za Mungu kwako. Kwa hiyo kama unataka kufurahia yale mengi ambayo Mungu ameweka kwa ajili yako basi hauna budi bali kuenenda katika Imani na upendo kwa watu wote. Barikiwa.

  • UMUHIMU WA IMANI

    “ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.”

    Waebrania 6:12

    Unajua katika ulimwengu wa biashara kinachotofautisha bidhaa bora na nyinginezo, ni faida anayoipata mtumiaji, na ndio maana kuna baadhi ya bidhaa hata kama ni za gharama kubwa kiasi gani lakini bado huwa hazikosekani majumbani mwetu, na yote ni kwa sababu tu ya  faida zake kwetu.

    Vivyo hivyo na kumpokea YESU kuna faida zake katika maisha yetu ya kila siku, baadhi ya faida zake huyu YESU ni uponyaji wa magonjwa na baraka tele. Sasa japokuwa kuna faida nyingine nyingi sana ukiacha hizo mbili zilizotajwa hapo juu, lakini watu wengi hawanufaiki na faida hizo, na sababu kuu ni kukosa Imani.

    Na ndio maana neno likasema

    “ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa IMANI na uvumilivu.”

    Waebrania 6:12

    Mtu wa Mungu kuna faida nyingi ndani ya Yesu, faida ambazo zinaweza kufanya maisha yako yakawa ya furaha na mafanikio hapa duniani lakini itakugharimu kuishi kwa Imani. Kumbuka neno la Mungu linasema kuwa

    “Mwenye haki ataishi kwa Imani……. Rumi 1:17” Barikiwa.

  • NAMNA YA KUMPENDEZA MUNGU

    “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”

    Waebrania 11:6

    Kama kuna jambo la muhimu sana kwetu kama Watoto wa Mungu basi litakuwa ni kuishi maisha yenye kumpendeza yeye (yaani Baba yetu wa Mbinguni).  Na ndio maana yeye (Mungu) hutufundisha neno lakekila wakati, makusudi tujue ni nini haswa yeye anategemea sisi tufanye ambacho kitamfurahisha.

    Lakini katika kutaka kupata muongozo zaidi kwa swala hili, basi andiko la utangulizi limeweka bayana kuwa kama tunataka kuishi maisha yenye kumpendeza Mungu basi ni lazima tuishi kwa Imani “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza…… Ebrania 11:6”

    Na kama tulivyotangulia kusema katika masomo yaliyopita tunapoongelea, kuishi kwa Imani tumesema ni kuishi kwa kufuata muongozo wa neno la Mungu katika kila jambo, yaani kuishi kwa kufuata nini maandiko yanelezea katika kila maamuzi na kisha ndio maamuzi yafanyike.

    Kwa hiyo shujaa wa Bwana hakikisha katika kila jambo unazingatia neno la Mungu linasemaje kuhusiana na hilo unalotaka kufanya na kisha fuata maelekezo yake, maana hayo ndio maisha ya Imani na yenye kumpendeza Mungu.

  • JINSI IMANI INAVYOFANYA KAZI

    “Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena;”

    2 Wakorintho 4:13

    Ni dhahiri kuwa kwa kusoma andiko la utangulizi utaona kuwa kuna uhusiano kati ya kuamini na kukiri unachoamini. Tena nikikurudisha nyuma kidogo kwenye namna tulivyopata wokovu, utagundua kuwa ulisimamia neno hili “ Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu….Rumi 10:10” .

    Kumbe sasa ni dhahili kuwa kwanza kabisa ili Imani ifanye kazi ni lazima ianzie rohoni kwa kuliamini neno lakini pili ni kuanza kukiri hilo neno.

     Hizi hatua mbili ni muhimu sana maana huwa zinaongozana kila mara katika utendaji kazi wa Imani.Kwa hiyo kama unataka Imani yako ifanye kazi ipasavyo basi fuata hatua hizi mbili nyepesi :

    1. Tafuta andiko la kusimamia ambalo linatoa muongozo wa namna ya kutatua changamoto yako

    Baada ya kuliombea hilo tatizo lako anza kukiri ushindi sawasawana andiko unalosimamia

  • CHANZO CHA IMANI

    “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”

    Rumi 10:17

    Kuna msemo usemao kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha, hii ni kuonesha kuwa kila jambo hata liwe kubwa namna gani bado lilianzia sehemu fulani na lilianzia likiwa dogo. Na Imani vivyo hivyo huwa na mwanzo wake japo ni mdogo lakini ndio chanzo cha mambo makubwa. Kwa kuangalia andiko la utangulizi utagundua chanzo cha Imani ni neno la Mungu.

    Yaani jinsi unavyozidi kulisikia neno la kweli basi ndivyo unavyozidi kukua katika Imani. Kwa hiyo shujaa wa Bwana kama unataka Imani yako ikue kiasi cha kukuwezesha kufanya mambo makubwa basi hakikisha kuwa unasoma neno la Mungu kila siku na kupata mafundisho yenye kujenga Imani yako mara kwa mara. Na kwa kufanya hivyo utakuwa umejihakikishia kukua katika wokovu. Barikiwa.

  • MWENYE HAKI NA IMANI

    “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.”

    Rumi 1:17

    Kutokana na andiko la utangulizi tunajifunza kumbe maisha ya mtu wa Mungu yanatakiwa kuongozwa na imani, yaani iwe ni kuhusiana na afya, Uchumi au hata hekima ya kufanya maamuzi mbalimbali bado tunatakiwa kuyafanya kwa Imani. Na tukirejea masomo ya nyuma tulisema kuwa Imani ni kuwa na UHAKIKA na neno la Mungu kwamba litafanya kama lilivyo ahidi.  Sasa kwa kuoanisha tafsiri ya Imani na andiko la utangulizi utagundua kumbe tunaposema kuishi kwa Imani haswa tunamaanisha kuishi kwa kufuata muongozo wa neno la Mungu. Iwe ni katika afya, uchimi au jambo lingine lolote ni muhimu kuzingatia neno la Mungu linasemaje kwanza kisha ndio uchukue hatua kuhusiana na changamoto yako.

    Shujaa wa Bwana maisha ya Imani ndio maisha yanayompendeza Mungu, maana ndio maisha ambayo yanamruhusu yeye kuhusika moja kwa moja na wewe, kwa hiyo ishi kwa Imani, ishi kwa kufuata neno la Mungu. Barikiwa.

  • MAANA YA IMANI

    “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”

    Ebrania 11:1

    Tokea ulipozaliwa mpaka sasa ninajua kuwa utakuwa umekutana na mafundisho mengi kuhusiana na mambo ya maisha, mfano ulipokuwa mdogo ulifundishwa kuwaita majina mbalimbali ndugu wa karibu na wazazi yaani huyu kuitwa mjomba,dada,mama au hata baba. Lakini je umewahi kujiuliza kipindi unafundishwa hayo yote kuna Ushahidi wowote ulipewa wa kuthibitisha hayo majina? Hakika jibu ni Hapana lakini bado wewe ULIAMINI na ndio maana hata leo unaendelea kuwaita kwa majina yao.

    Hivyo ni sahihi kusema kuwa Imani ni kuwa na uhakika juu ya yale yasiofahamika au kuonekana kwa sasa. Na kwa vile tunajifunza Imani itokanayo na neno la Mungu basi tunaweza kutafsiri Imani kwa namna hii “IMANI ni kuwa na uhakika na neno la Mungu kuwa litafanya (yale yasioonekana au kufahamika kwa sasa) kama vile lilivyo sema”.

    Kwa hiyo mtu wa Mungu kama ulikuwa ufahamu basi kuanzia sasa ndio ujue kuwa Imani ya kweli ni kuwa na uhakika na neno la Mungu kwamba litafanya kama vile lilivyosema, na kwa mantiki hiyo kama unakutana na changamoto yoyote basi anza kwa kutafuta neno la Mungu linasemaje kisha simamia hilo neno katika maombi mpaka utakapo pata majibu yako. Barkiwa.

  • TUNASHINDA KATIKA YOTE

    “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”

    Rumi 8:37

    Hakuna mtu anaweza kuzuia changamoto zisije, maadamu upo duniani basi utakutana nazo tu. Hivyo ni busara kujua basi ni namna gani unaweza kuzishinda. Maana andiko linatuonesha kuwa “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye” kumbe ni katika Yesu tunashinda mambo yote yaani tunapata utatuzi wa kila changamoto. Ngoja nikuambie kitu shujaa bwana hakika Mungu ametupendelea sana, maana kwa kutupatia jina la Yesu ni kama kusema ametupa uhakika wa kushinda katika kila jambo. Wewe kazi yako ni kuitilia jina la Yesu katika tatizo lako na Mungu ataingilia kati na kukupa ushindi. Kwa hiyo mwana wa Mungu usikubali kuonewa na shetani wewe simama katika maombi, endelea kuliitia jina la Yesu maana ni katika yeye tunapata ushindi. Barikiwa.

  • KWA YEYE TUMEPATA NEEMA

    “ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.”

    Rumi 5:2

    Neema ni haki ambayo mtu hupokea, sio kwa sifa binafsi bali kwa kupewa yaani ni kwa upendeleo. Sisi sote hatukuwa na haki ya kuitwa wana wa Mungu ila ni kwa neema zake Mungu tu tumepata fursa hiyo. Na kwa kuwa sasa tumeitwa wana wa huyu Mungu aliye hai, moja kwa moja tuna haki ambazo tumezipokea kutoka kwake. Haki kama vile ya kuponywa magonjwa (Isaya 53:5), haki ya kupata msaada wa kiuchumi ( wafilipi 4:19)  na haki nyinginezo nyingi.

    Kwa hiyo shujaa wa bwana simama katika zamu yako na udai kilicho chako, maana ni haki yako kuishi maisha ya furaha yenye baraka tele kwa sababu wewe ni mwana wa Mungu. Barikiwa.

  • MUNGU AKUPAYE KUFANIKIWA

    “Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake.”

    Zaburi 35:27

    Mungu ninaye muamini na kutangaza habari zake ni mwema sana, yeye sio kama miungu mingine ya duniani hapa ambayo huwalipa watu wake mabaya badala ya mema kwa kuwatumikia. Ila ni kinyume chake, Mungu wetu huwalipa watu mema kila wakati hata katika nyakati ambazo huwa tunashindwa kuishi kama ipasayo na tukaanguka kwa bahati mbaya bado Mungu hutulipa mema na kutuonesha rehema zake tele.

    Na ndio maana maandiko yanatuonesha kuwa na “Atukuzwe Mungu“ kwa kuwa yeye amestahili sifa kwa hakika.

    Na sasa Habari njema ni kuwa huyu Mungu ambaye ni mwingi wa rehema, yeye anapenda kukufanyia mambo mema. Na ndio maana anasema kuwa yeye hufurahishwa na Amani yangu na yako. Kwa iyo shujaa wa bwana endelea kumuamini huyu Mungu na kufurahia wingi wa rehema zake. Barikiwa.

Design a site like this with WordPress.com
Get started